News

UGANDA: MAMIA YA MAHUJAJI WAANZA KUTEMBEA KWA MIGUU KUELEKEA NAMUGONGO.

on

Mamia ya mahujaji wa kikristo nchini Uganda na maeneo jirani, tayari wameanza safari yao ya hija, kuelekea katika kuadhimisha kumbukumbu ya mashahidi wa Uganda mnamo Juni 3.

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari nchini humo, watu kutoka maeneo mbalimbali, wameanza safari ya hija yao kuelekea Namugongo-Kampala, ambako ndiko hufanyika hija ya kuwakumbuka mashahidi wa Uganda, walio kubali kutoa maisha yao kwa ajili ya mkombozi wao Yesu Kristo.

Miongoni mwa walioripotiwa kuanza safari, ni pamoja na kundi la mahujaji kutoka Gulu, Kaskazini mwa Uganda, ambao hadi sasa wameweza kutembea mwendo wa kilomita 30 tu, kati ya 360 zilizopo kutoka Gulu hadi Kampala.

Mwaka hadi mwaka, waumini hawa wamekuwa wakitembea kwa miguu toka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nje ya nchi ya Uganda, ikiwa inaaminika kuwa, sadaka ya mateso wanayoipata watu hawa, ni sehemu ya kumbukizi ya mateso waliyo yapata mashahidi wa hao.

Hata hivyo, mahujaji hao hukumbana na changamoto nyingi njiani, kama vile kunyeshewa na mvua, kuishiwa chakula, kukosa nguvu za kuendelea na safari kwa baadhi yao na mengine ya kurandana na hayo, kwani hulazimika kutembea kwa muda mrefu na kwa mwendo mrefu sana.

Mashahidi wa Uganda ni kundi la watu 23 wa kanisa la Anglikani pamoja na 22 wa kanisa Katoliki katika historia ya ufalme wa Buganda, ambao ni sehemu ya nchi ya Uganda, walio uwawa kati ya Januari 31, 1885 na 27 Januari 1887, kutokana na amri ya Mwanga II, mfalme wa Buganda.

*Baadhi ya mahujaji wakitembelea yalipo makumbusho ya mashahidi wa Uganda.*

Mauaji hayo yalitokea wakati ambao kulikuwa na mvutano wa kidini, ambao ulikuwa ukisababishwa na shinikizo la kisiasa katika mahakama ya kifalme ya Buganda.

Kanisa Katoliki, kanisa la Anglikani pamoja na waumini wa dini ya kiislam, walijikuta katika mgogoro mzito wa vuta n’kuvute ya nani aliye zaidi ya mwingine, ambao ulipelekea mfalme Mwanga II kuamuru kuuwawa kwa baadhi ya waumini wa dini ya kikristo.

Mnamo Juni 3, kanisa Katoliki pamoja na la Anglikani nchini Uganda, yatakuwa yanaadhimisha kumbukizi ya mashahidi hao wafia dini, ambapo maelfu ya watu wanatarajiwa kukusanyika Namugongo kutoka sehemu mbalimbali, ambapo ndipo yalipo makumbusho ya mashahidi hao.

 

Please follow and like us:
0

About Linuce Libent

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Translate »
WhatsApp chat