News

NEWS: KAMPALA-UGANDA; UHABA WA MVUA; WAFANYA BIASHARA WAONYWA KUTOKUUZA MAZAO YA CHAKULA NJE YA NCHI.

on

Serikali nchini Uganda imewatahadharisha wafanya biashara, kutokuuza mazao ya chakula nje na nchi hiyo. Hii ni kutokana na kuzidi kukosekana kwa mvua za kutosha, ambapo wasiwasi wa kuzidi kuwa na ukame bado ni mkubwa na hivyo kutakiwa kukihifadhi chakula kilichopo kwa umakini mkubwa.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Uganda pamoja na nchi jirani kama vile Ethiopia, Kenya, Somalia na Sudani ya Kusini, zimeshuhudia madhara makubwa ya ukame ambayo ni vifo vya watu, mifugo pamoja na kukosekana kwa maji na chakula cha kutosha.

Tangu mwenzi wa 11 mwaka Jana, Uganda imekuwa na tatizo la ushukaji wa uchumi, ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uzalishaji mdogo uliopo katika sekta ya kilimo, kutokana na hali ya hewa kuwa ni ukame.

Hivi karibuni, mamlaka ya hali ya hewa nchini humo, imetoa angalizo kutokana na kutegemewa kuchelewa kunyesha kwa mvua katika maeneo mengi, jambo ambalo ni kinyume na ilivyokuwa kawaida, kwani kuanzia mwezi wa 3 imezoeleka kuwa ni msimu wa mvua katika maeneo yaliyo mengi, lakini imekuwa ni tofauti kwa mwaka huu hadi sasa.

Hivyo, kutokana na taarifa hiyo, serikali imewataka wafanya biashara kuuza mazao yao ndani ya nchi, hasa katika maeneo ya Kaskazini mwa Uganda pamoja na Karamoja ambako uhaba wa chakula ni mkubwa sana.

Waziri wa nchi wizara ya kilimo Bwana Christopher Kibanzanga, amesema kuwa, si vyema kwa wafanya biashara kuuza chakula nje ya nchi huku maelfu ya watu nchini humo wakiwa hawana chakula. Pia ameongeza kuwa, hali hii inategemewa kuzidi kuathiri hadi ngazi ya familia, kutokana na uhaba wa vyakula, kupanda kwa bei ya vyakula pamoja na kuporomoka kwa uchumi.

Ikiwa mvua zitaendelea kukosekana; zaidi ya watu milioni 10 kutoka katika nchi za Afrika Mashariki wapo hatarini kupatwa na baa la njaa, kwani kuzidi kukosekana kwa mvua, kutaendelea kusababisha ukosekanaji wa uzalishaji wa mazao ya chakula.

Please follow and like us:
0

About Linuce Libent

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Translate »
WhatsApp chat